Wananchi wa kata ya Kate wakimsikiliza
Mkuu wa wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
KATIKA harakati za kupambana na migogoro kati ya Wakulima na
Wafugaji wilayani Nkasi serikali inatarajia kuanzisha sensa ya mifugo ili kujua
idadi ya mifugo iliyopo kulinganisha na ukubwa wa eneo la wilaya na kuwa mifugo
itakayozidi itabidi iondolewe.
Akizungumza na Wananchi kwenye mikutano ya hadhara jana
katika kata za Sintali,Myula na Kate mkuu wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Said
Mohammed Mtanda alisema kuwa viashiria
vya migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji vimeanza kutokea wilayani humo na
kuwa suluhisho ni kuwa na mifugo inayolingana na ukubwa wa eneo la wilaya.
Alisema inaonekana sasa mifugo katika wilaya Nkasi ni mingi
ukilinganisha na eneo la malisho lililopo na kuwa suluhisho ni kufanya sensa ya
mifugo ili kujua idadi ya mifugo iliyopo kulinganisha na eneo la malisho
lililopo na kuwa kama ikibainika mifugo ni mingi ile iliyozidi itabidi
iondolewe katika wilaya
Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa anazo taarifa kuwa baadhi ya
viongozi wa vijiji wamekua wakipokea rushwa kutoka kwa Wafugaji na kuwaruhusu
kuingiza mifugo katika vijiji vyao kinyume cha sheria bila ya kukubalia na
wananchi na bila ya kuangalia ukubwa wa eneo la malisho.
Hivyo amewataka viongozi wa vijiji ambao walipokea fedha za
rushwa ili kuwakaribisha wafugaji hao kinyume cha sheria katika vijiji vyao
kuzirudisha fedha hizo kabla ya sensa hiyo haijaanza na kuwataka wafugaji ambao
walitoa rushwa kwa watendaji wa vijiji ili waingize mifugo katika vijiji vyao
watoe taarifa kwake mara moja ili aamuru fedha zao zirudishwe na kuondoa mifugo
yao katika vijiji hivyo mara moja
‘’taarifa nilizonazo mifugo katika vijiji vyenu ni mingi
kuliko idadi ya watu na wengi wameingiza mifugo yao katika vijiji vyenu kwa
kutoa rushwa kwa viongozi wa vijiji sasa sensa hiyo itatupatia majibu halisi
juu ya idadi ya mifugo iliyopo na watatuambia waliingieje katika vijiji hivi’’alisema
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewataka Wananchi
wa vijiji hivyo kuwasilisha kero mbaimbali wanazokumbana katika vijiji vyao
badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa wanapofika na kuandika mabango wakati
kero zao zingeweza kutatuliwa na uongozi wa wilaya.
Alisema kuwa kama kuna mtu hajapata huduma sitahiki kwenye
ofisi ya serikali asisite kutoa taarifa haraka kwenye ofisi yake ili mradi tu taarifa hizo ziwe ni
za kweli atachukua hatua za haraka kuwawajibisha wale wote watakaokwenda
kinyume na utumishi wa Umma na kuwa si vizuri kusubiri viongozi wa kitaifa kama
Rais,Waziri mkuu na Makamo wa Rais kumweleza matatizo wakati ofisi ya mkuu wa
wilaya haijashindwa kutatua hilo na kuwataka kujenga utamaduni huo wa
kuifikishia serikali ya wilaya zile changamoto wanazozipata.
Bw,Mtanda aliwataka pia wananchi kuanzia sasa kuwa na Banki
ya matofali kuanzia sasa katika vijiji vyao ambayo yatatumika katika kufanyia
shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na
maendeleo mengine.
Wananchi pia waliweza kumweleza kero mbalimbali walizonazo
ambapo nyingine zilitatufutiwa ufumbuzi wa papo hapo
mwisho
|
No comments:
Post a Comment